Sunday, February 26, 2012

Walioshindwa mbinu

Mbinu walioishiwa, wepesi kukimbilia,
Fujo kuzichochea, wavune yanayowafaa,
Ukubwa kuutetea, japo waisha raia,
Walioshindwa mbinu, mikakati na fikra:
Mabavu huyatumia!

Ni watu wa kuteua, watu wasiowafaa,
Yao waangalia, si ya wengi yakawa,
Ni laana tumeachiwa, bado tunaing'ang'ania,
Walioshindwa mbinu, mikakati na fikra:
Mabavu huyatumia!

Enzi za kutofikiria, ukingoni zafikia,
Watu wataulizia, hata yale yasokuwa,
Na wajibu kuwatia, wajifanyao wajua,
Walioshindwa mbinu, mikakati na fikra:
Mabavu huyatumia!

Majoho watawavua, yafichyo kuishiwa,
Ujinga wakawaachia, na wengine kuchagua,
Pasiwe wa kubakia, na mtu anayetumiwa,
Walioshindwa mbinu, mikakati na fikra:
Mabavu huyatumia!

No comments: