Wednesday, February 22, 2012

Watu wetu ndio nchi

Watu wetu ndio nchi, vinginevyo haijawa,
Tukiwageuzia mchi, kitu gani twabakiwa,
Hii sasa ngumu mechi, wengi sana wanapwaya,
Siasa ilivyokuwa, hazinao mwelekeo:
Chochote chaweza kuwa,
Si gamba tu kujivua,
Wengine wa kung'olewa!

Nchi wanaichezea, mfukoni waloia,
Viongozi walokuwa, japo mwalimu kaonya,
Na wote wanajijua, unafiki wajitia,
Siasa ilivyokuwa, hazinao mwelekeo:
Chochote chaweza kuwa,
Si gamba tu kujivua,
Wengine wa kung'olewa!

Nchi ukiiachia, mamboye bila kujua,
Lolote weza tokea, hadi likakushtua,
Hivi tunayaelewa, chini wanayojifanyia?
Siasa ilivyokuwa, hazinao mwelekeo:
Chochote chaweza kuwa,
Si gamba tu kujivua,
Wengine wa kung'olewa!

Tunayo teknolojia, twaweza kuitumia,
Ikawa tunayajua, mawaziri kufatia,
Makatibu kwangalia, wendayo kila hatua,
Siasa ilivyokuwa, hazinao mwelekeo:
Chochote chaweza kuwa,
Si gamba tu kujivua,
Wengine wa kung'olewa!

Na wakuu wa mikoa, wajifunzao wakiwa,
Kazini wameshaingia, yote yao ukajua,
Na wakuu wa wilaya, kuwadhibiti ikawa,
Siasa ilivyokuwa, hazinao mwelekeo:
Chochote chaweza kuwa,
Si gamba tu kujivua,
Wengine wa kung'olewa!

Kompyuta huangazia, yao ndani yakatiwa,
Kitufe kikishabonyea, taarifa waitoa,
Pasiwe la kushtua, maana yote wajua,
Siasa ilivyokuwa, hazinao mwelekeo:
Chochote chaweza kuwa,
Si gamba tu kujivua,
Wengine wa kung'olewa!

Nchi isije nunuliwa, nawe kamba washikilia,
Kama Dowans ilivyokuwa, mkenge watu kuingia,
Nao wakakubishia, nchi yao imeshakua,
Siasa ilivyokuwa, hazinao mwelekeo:
Chochote chaweza kuwa,
Si gamba tu kujivua,
Wengine wa kung'olewa!

Kariakoo yatokea, Ikulu kutokujua,
Wazee wasanzuliwa, wageni nyumba watwaa,
Kila mtu ayajua, nasi tunaangalia,
Siasa ilivyokuwa, hazinao mwelekeo:
Chochote chaweza kuwa,
Si gamba tu kujivua,
Wengine wa kung'olewa!

Mifumo inatakiwa, mambo kufuatilia,
Kila wakati kujua, nini kinahoendelea,
Mabaya kutokutokea, na harufu kuwa mbaya,
Siasa ilivyokuwa, hazinao mwelekeo:
Chochote chaweza kuwa,
Si gamba tu kujivua,
Wengine wa kung'olewa!

Ndiwe twakukusudia, Azizi uliyekuwa,
Mwingi wa kutujalia, na mabaya kutwepushia,
Tuonyeshe njema njia,iokoke Tanzania,
Siasa ilivyokuwa, hazinao mwelekeo:
Chochote chaweza kuwa,
Si gamba tu kujivua,
Wengine wa kung'olewa!

No comments: