Monday, February 20, 2012

Msigeuze mazishi

Wachawi pia walozi, sherehe zao mazishi,
Hili muhimu zowezi, linavuta matoashi,
Haifanyiki ajizi, kuukuza ushawishi,
Msigeuze mazishi, kuwa fashioni shoo!

Na walokuwa wajuzi, huzisafisha burashi,
Wawapake wenye enzi, wanaoidai arshi,
Kama kufa hawawezi, yakawa yao mazishi,
Msigeuze mazishi, kuwa fashioni shoo!

Kiafrika ni majonzi, maziko kuwa nakshi,
Mbona wetu hatuenzi, wakati wanapoishi,
Haya ni gani mapenzi, naona yote uzushi,
Msigeuze mazishi, kuwa fashioni shoo!

Yafanyeni mashauzi, kuliko na matapishi,
Huko kusiko na kazi, ila udariweshi,
Wa kujitia wazuzi, kumbe wote ni wazushi,
Msigeuze mazishi, kuwa fashioni shoo!

Mnajitia wakwezi, kumbe nanyi kinamashi,
Mwajitia viongozi, hali wote magumashi,
Waibao kama njozi, kwa ngazi za kashikashi,
Msigeuze mazishi, kuwa fashioni shoo!

Chetu mnajipa hadhi, kuwa chenu mkagushi,
Na walio waandazi, wajifanya ni wapishi,
Wasio nao ujuzi, kujifanya matarishi,
Msigeuze mazishi, kuwa fashioni shoo!

Umezidi udowezi, nchi yenye bakshishi,
Hivi tuna viongozi, asu sasa matoashi?
Mbona zazidi ajizi, na kauli za uzushi?
Msigeuze mazishi, kuwa fashioni shoo!

Ngoma hii hamuwezi, mnakuwa matapishi,
Wageni nao wakazi, wawaona mafurushi,
Mizigo isiyo kazi, kubebwa bila ubishi,
Msigeuze mazishi, kuwa fashioni shoo!

No comments: