Wednesday, February 1, 2012

Mvi koja la uzee

SI busara si hekima, mvi koja la uzee,
Kula aliye adhama, nafusi aifungue,
Ni muda wa kujituma, mema watu uachie,
Mvi koja la uzee, si akili si hekima!

Si muda wa kujinoma, wengine uwazuie,
Na madhambi kuchuma, kwa kutaka chako kiwe,
Na wengine kuwazima, upendacho wasitwae,
Mvi koja la uzee, si akili si hekima!

Wakati wa kuegema, ulozua uezue,
Ukapunguza hasama, na Mola umwagukie,
Ukitafuta rehema, si vigumu ugawiwe,
Mvi koja la uzee, si akili si hekima!

Ni wakati wa kusoma, usojua uyajue,
Kisha upange kalima, wengine uwaambie,
Kwa vitabu kujituma, tini uwachapishie,
Mvi koja la uzee, si akili si hekima!

Ni wakati wa kuhama, ya dunia uambae,
Na imani kuifuma, zaidi ikunyanyue,
Na mbali ukatazama, ya ghaibu uyajue,
Mvi koja la uzee, si akili si hekima!

Tamaa huwa kilema, ikifikia uzee,
Huibuki utazama, bwawani utumbukie,
Ikawa huonekani, hata watu wazamie,
Mvi koja la uzee, si akili si hekima!

Husoma mwenye hekima, alama azitambue,
Wakati wenye uzima, ya kwake ajifanyie,
Na taa zinapozima, kitandani aingie,
Mvi koja la uzee, si akili si hekima!

Uzee si kulalama, maumivu yapungue,
Uzee kubwa heshima, ibadani ubakie,
Pumzi zako ghanima, kwa dua uongezee,
Mvi koja la uzee, si akili si hekima!



Februari 1, 2012
Dar es Salaam

No comments: