Saturday, February 18, 2012

Dereva wenu mjinga

Atamba na gari dogo, suka wenu hamnazo,
Vipi kibanzi ba gogo, kuingia kwenye mzozo?
Wajua hata Wagogo, kibanzi hana uwezo,
Dereva wenu mjinga, atamba na gari dogo?

Msasani na Kigogo, pasiwe nayo mabezo,
Wa kwanza ni mkorogo, wa pili ni maumbizo,
Hupata aso msago, wa msago awe uozo,
Dereva wenu mjinga, atamba na gari dogo?

Angehofia kipigo, asingezua mzozo,
Pengine huyu Mdigo, ubishi kwao mwongozo,
Huliacha lao chago, kwenda ona maigizo,
Dereva wenu mjinga, atamba na gari dogo?

Unguja huitwa chogo, Mnyamwezi bila nguzo,
Hawahitaji mabago, hili la bure tangazo,
Kwao kubwa huwa dogo, na dogo likawa ZOZO,
Dereva wenu mjinga, atamba na gari dogo?

Ninazichelea figo, kuchekwa kwangu kikwazo,
Kicheko changu magego, na upepo mapulizo,
Na huu sio mtego, na wala sio kibonzo,
Dereva wenu mjinga, atamba na gari dogo?

Atapowika jogoo, kwako isiwe shangazo,
Dua yake sio ndogo, malaika ni mzomzo,
Omba yaliyo kiwango, hupewa lako ombezo,
Dereva wenu mjinga, atamba na gari dogo?

No comments: