Monday, February 20, 2012

Kwa shani wanaozuka

Hawaachi kuzuzuka, wanaozuka kwa shani,
Sanaa wanapovuka, hudhani wana thamani,
Wajione watukuka, nyumbani na mitaani,
Wanaozuka kwa shani, hawaachi kuzuzuka !

Kichwani yakishafika, wengi huwa ulevini,
Wajione wamefika, nao bora duniani,
Wakasahau hakika, hapa tuko mitumbani,
Wanaozuka kwa shani, hawaachi kuzuzuka !

Akili huwalipuka, wakawa ni majinuni,
Wakafanza ya dhihaka, wakacheka wanandani,
Washeshimu na rika, kujifanya baniani,
Wanaozuka kwa shani, hawaachi kuzuzuka !

Na shule ikipingua, usanii wawa guni,
Hawana watolojua, ila kidogo imani,
Wao wakajidhania, waifanya ihsani,
Wanaozuka kwa shani, hawaachi kuzuzuka !

Huchupa wakachupia, warudi abautani,
Huruka kujinyanyua, tahamaki wako chini,
Hupinda wakapindua, wasiwe barabarani,
Wanaozuka kwa shani, hawaachi kuzuzuka !

Hushika wakaachia, wakashika vya utani,
Kuja kushitukia, hakuna kitu mkononi,
Hujikweza wakakwea, ghorofa za kuelea,
Wanaozuka kwa shani, hawaachi kuzuzuka !

Wakija kushtukia, huporomoka chini,
Moja ikija balaa, hujikuta nuksani,
Na waliowazimia, wawafanze afkani,
Wanaozuka kwa shani, hawaachi kuzuzuka !

Matope watu hupaka, huku eti wahisani,
Haya yakijasikika, hujikuta maruhani,
Nguvu kuja ishiwa, utu ukawa shimoni,
Wanaozuka kwa shani, hawaachi kuzuzuka !

Kila kitu watataka, na kujipa ya thamani,
Wadharau walikotoka, wenyeji kuwa wageni,
Tapeli wanakotoka, wakaonekana shani,
Wanaozuka kwa shani, hawaachi kuzuzuka !

Aya zimekusanyika, ametuonya Manani,
Dini wasioitaka, si fungu la duniani,
Na akhera wakifika, huwa wageni motoni,
Wanaozuka kwa shani, hawaachi kuzuzuka !

No comments: