Wednesday, February 29, 2012

Midomo na maneno hayashindi !!!!

WATANZANIA shabashi, fundi wa kuzungumza,
Tabasamu na ucheshi, vichache wanaviweza,
Umebaki ushawishi, historia kujuza,
Tunacheza kwa mdomo, na wenzetu kwa mguu:
namna hii tutashinda ?

Usanii twabakia, kimichezo tumekwisha,
Na tuanowachagua, mazishi tunawatwisha,
Ujuaji ukikua, ndio mwisho wa maisha,
Tunacheza magazeti, na wenzetu kiwanjani:
hivi kweli tutashinda?

Mipango twaipangua, na siasa kuzitia,
Wataalamu twaachia, wazawa waliokuwa,
Na kwenda kuwavamia, watalii wa dunia,
Tunacheza kwa tivii, wenzetu kwa mikakati:
hivi kweli tutashinda?

Michezo yataka nia, mipango nazo hatua,
Viwanja ukaanzia, safi vilivyonakshiwa,
Vikatosheleza vifaa, mazoezi kufanzia,
Tunacheza kisiasa, wenzetu kiushindani:
hali hii tutashida ?

Majengo yanatakiwa, kwa michezo ya kulea,
Ndani inayotakiwa, uzio yakajengewa,
Kila kitu ndani kuwa, pasiwe kinachopungua,
Tunacheza kwa mdomo, na wenzetu kwa mguu:
namna hii tutashinda ?

Vifaa vinatakiwa, mbalimbali vilokuwa,
Navyo vya kununua, na kujitengenezea,
Ajira tunazichezea, wakati hakuna vifaa?
Tunacheza magazeti, na wenzetu kiwanjani:
hivi kweli tutashinda?

Walimu wanatakiwa, mizizi waliokuwa,
Mfano wao Zambia, na wa nje kukodiwa,
Ratiba kuiandaa, ya mwaka mzima ikawa,
Tunacheza kwa tivii, wenzetu kwa mikakati:
hivi kweli tutashinda?

Misitu inatakiwa, mazoezi kufanyia,
Ya kupanda na kutua, na wala sio asilia,
Mandhari kunyanyua, bora zilizojaliwa,
Tunacheza kisiasa, wenzetu kiushindani:
hali hii tutashida ?

Huko zana zikatiwa, pamwe na vyote vifaa,
Mtu aweza kukaa, siku nzima katulia,
Mazoezi kufanzia, hadi akajichokea,
Tunacheza kisiasa, wenzetu kiushindani:
hali hii tutashida ?

TFF huu kuwa, na sio kuingiliwa,
Na hao wanaojijua, wajua na wasiojua,
Talanta wakaishapewa, mwisho wa mwaka kuzaa,
Tunacheza kwa mdomo, na wenzetu kwa mguu:
namna hii tutashinda ?

Vijiweni twaingia, na soka kujichezea,
Timu tukajipangia, ushindi kuja chukua,
Uwanjani wakitua, nguo zote wavuliwa,
Tunacheza kwa mdomo, na wenzetu kwa mguu:
namna hii tutashinda ?

Magazeti Tanzania, namba wani yamekuwa,
Yacheza kama Zambia, kwa maneno kuyatoa,
Na kisha kujishangilia, uwanjani bado tua,
Tunacheza kwa mdomo, na wenzetu kwa mguu:
namna hii tutashinda ?

Kucharangwa hufatia, wote kimya wakawa,
Kama wangelijua, ni mbali wangeanzia,
Maandalizi kwingia, wahamasishe kwa nia,
Tunacheza magazeti, na wenzetu kiwanjani:
hivi kweli tutashinda?

Mazoezi kufatia, ndani na nje yakiwa,
Hadi timu kujaliwa, viwango ikafikia,
Na kisha kuhesabia, vile vinavyotakiwa,
Tunacheza kwa tivii, wenzetu kwa mikakati:
hivi kweli tutashinda?

Wazee kuwaondoa, wakati umewadia,
Timu mpya kuzaliwa, vishindo kuhimilia,
Kila siku twawajua, hawa waliojichokea,
Tunacheza kisiasa, wenzetu kiushindani:
hali hii tutashida ?

Mbona kubwa Tanzania, na thelathini mikoa,
Twashinda kujipatia, kumi na moja walokuwa,
Bora na wa kidunia, tuionyeshe dunia?
Tunacheza kisiasa, wenzetu kiushindani:
hali hii tutashida ?


Februari 29, 2012
Sudusia (1/6) ya 2012.
Dar es salaam. Tanzania.

No comments: