Monday, February 20, 2012

Hivi wezi na warongo ... ?

Kuna tulipokosea, kwa waovu kuachia,
Tukawa twatarajia, uhai kutuchunia,
Na haki kutupigania, zisiwe zanunuliwa,
Hivi wezi na waongo, waweza linda raia ?

Dola safi yatakiwa, uchamungu wanajua,
Si watu wenye tamaa, na mali kuzikamia,
Wengi twenda kuumia, hawa tukiwaachia,
Hivi wezi na waongo, waweza linda raia ?

Na wakubwa walokuwa, wakiwatumia vibaya,
Wakaamuru ubaya, raia kuwatendea,
Kichwa chao kinakuwa, na misuli kujitia,
Hivi wezi na waongo, waweza linda raia ?

Na mwisho tukigundua, nchi imeshapotea,
Magenge yakutuua, wenyewe tukayazua,
Kila mwenye fedha akawa, aweza kuwanunua,
Hivi wezi na waongo, waweza linda raia ?

Italia Tanzania, wezi viongozi kuwa,
Lolote wataamua, iwapo kwao yafaa,
Pasiwe na manufaa, ila ni kujijutia,
Hivi wezi na waongo, waweza linda raia ?

Wenzangu nawaambia, katiba kuiangalia,
Vifungu kuamuliwa, kazi linazopembua,
Kuwapata wanaofaa, si kuajiri balaa,
Hivi wezi na waongo, waweza linda raia ?

No comments: