Monday, February 20, 2012

Kweli akili hazina, ukiritimba kwa leo!

Ni nani kakuambia,ujinga umeenea,
Akili tumejaliwa, kila mtu huzaliwa,
Ukiwa hili wajua, mwenzio lile ajua,
Kweli akili hazina, ukiritimba kwa leo!

Tofauti inakuwa, kwa kile unachojua,
Na wanaojidhania, kila kitu wanajua,
Nchi ndio wanaua, na maendeleo kuvia,
Kweli akili hazina, ukiritimba kwa leo!

Ni wakoma walokuwa, na washikacho hunywea,
Kikawa cha kudumaa, na sicho kinachokua,
Na haya yanatokea, nasi tunaangalia,
Kweli akili hazina, ukiritimba kwa leo!

Kula anayosomea, ubingwa akajaliwa,
Afaa akachiwa, kufanya analojua,
Kila tukiingilia, twazidi kuharibia,
Kweli akili hazina, ukiritimba kwa leo!

Siasa zinachafua, taasisi zilizokuwa,
Wasiojua wakwea, wasipopasaidia,
Na hali mbaya ikawa, kila siku kujongea,
Kweli akili hazina, ukiritimba kwa leo!

Walo juu watulia, uziwi umeingia,
Hakuna wa kusikia, nusura kuiamua,
Nchi yazidi fubaa, na rangi zinapotea,
Kweli akili hazina, ukiritimba kwa leo!

Si uchumi ni chomoa, namba zinavyotokea,
Kitu gani kikakua, huku chazidi dumaa?
Wananchi wanashangaa, ajabu iliyokuwa,
Kweli akili hazina, ukiritimba kwa leo!

Macho nimeyafungua, moyo nimejifungia,
Siwezi haya pokea, ujinga naukataa,
Ila nikishajionea, kesho itakavyokuwa,
Kweli akili hazina, ukiritimba kwa leo!

Februari 20, 2012
Dar es Salaam. Tanzania.

No comments: