Sunday, February 19, 2012

Mpira maandalizi

Haiwi, haitakuwa, kushinda kwa kukamia,
Muache kujiandaa, ushindi mkachukua,
Mpira wataka nia, na malengo kupembua,
Mwategemea ushindi, kiwango hamjafikia!

Mapambo kujipambia, si ushindi kuingia,
Kelele hazitofaa, kama unachechemea,
Na mgonjwa haijawa, kumshinda muafua,
Mwategemea ushindi, kiwango hamjafikia!

Mipango pa kuanzia, na kisha kumalizia,
Uongozi ulokuwa, meneja wakafuatia,
Na kocha akaachiwa, kufanya anayojua,
Mwategemea ushindi, kiwango hamjafikia!

Haiwa, haitakuwa, michezo kuendelea,
Huku mnaichezea, na mengine ya udhia,
Nani atajaliwa, hali kama hii 'kiwa?
Mwategemea ushindi, kiwango hamjafikia!

Watunzi mwawatukia, na mashairi mwabeua,
Laiti mngelijua, hazina iliyokuwa,
Hawa mngewaingia, ushauri mkapewa,
Mwategemea ushindi, kiwango hamjafikia!

Hamuwezi itania, sanaa iloridhiwa,
Watu inayoongoa, na usafi kuingia,
Inayofuta madoa, weupe ukapagawa,
Mwategemea ushindi, kiwango hamjafikia!

Vichaa mwaangaliwa, mambo mnavyojifanzia,
Laana zawatambaa, kwa janaba zilokuwa,
Nani wa kuwaridhia, wasafi msipokuwa?
Mwategemea ushindi, kiwango hamjafikia!

Wachache waliokuwa, sio wote tunajua,
Hawa yafaa kutoa, watu safi kuopoa,
Ni mwanzao kufanikiwa, vinginevyo mwatania,
Mwategemea ushindi, kiwango hamjafikia!

Sijali mwanisikia, au mnashangilia,
Michezo sasa udhia, hata siku za kujia,
Naam tutajionea, nako huko Britania,
Mwategemea ushindi, kiwango hamjafikia!




Tanzania namba moja

Namba moja Tanzania, mdomo kuuchezea,
Mpira wawakataa, walazimisha ulua,
Vigumu kuendelea, bila ya kujiandaa,
Tanzania namba moja, kwa mpira wa mdomo!

Vijana wanatakiwa, toka kote Tanzania,
Si kuwang'ang'ania, kilele walofikia,
Nchi nzima kutembea, vipaji kuviibua,
Tanzania namba moja, kwa mpira wa mdomo!

Magazeti yazuzua, tofauti inavyokua,
Kunyukwa ndiyo tabia, ushindi twausikia,
Kujifunza twalemewa, uwezo umetuishia?
Tanzania namba moja, kwa mpira wa mdomo!

Hata kwaya twaimbiwa, bado hazijaingia,
Ushindi twatabiriwa, ni kushindwa twaombewa?
Mipango hatujaijua, mchezo twautania,
Tanzania namba moja, kwa mpira wa mdomo!

Makocha wa kubabia, na viwanja vya udhia,
Lini itaondokea, ushindi tukajaliwa?
Ndumba, juju zimevia, soka guu latakiwa,
Tanzania namba moja, kwa mpira wa mdomo!

Hakika Watanzania, wameshiba kwa tamaa,
Ila haijatokea, ushindi bure kupewa,
Kazi kubwa yatakiwa, na pia kujiandaa,
Tanzania namba moja, kwa mpira wa mdomo!

Vijana kuwanyanyua, toka msingi wakiwa,
Na kisha kushindania, wilaya nayo mikoa,
Polepole wakikua, shule moja waingia,
Tanzania namba moja, kwa mpira wa mdomo!

Shule moja waingia, maalum kwendelea,
Vipaji vikalelewa, na soka lipate kua,
Huku watachaguliwa, timu zote kuingia,
Tanzania namba moja, kwa mpira wa mdomo!

Mvinyo maji wajaa, na sifa zisizopungua,
Ila kweli haitakuwa, hadi uvivu kutoa,
Na nia kuazimia, vitani kwenda ingia,
Tanzania namba moja, kwa mpira wa mdomo!

Na nia kuazimia, vitani kwenda ingia,
Ushindi mkautwaa, kiwanjani sio baa,
Maneno yakipungua, vitendo budi kukua,
Tanzania namba moja, kwa mpira wa mdomo!

Michezo ya Tanzania, kama nchi imekua,
Twapenda kujisifia, hata peke yakichipua,
Ndoto tunajiotea, nalo sijalikubalia,
Tanzania namba moja, kwa mpira wa mdomo!

Watu fedha wanaliwa, kwa vimeo kusifiwa,
Hilo litawaumbua, watu wakiwakimbia,
Kwanza viwango kupaa, kisha kujisifia,
Tanzania namba moja, kwa mpira wa mdomo!

Haijawa, haitakuwa, kushinda kwa kusifiwa,
Kitendawili tanzua, mitishamba si maua,
Akili asotulia, kushinda huwa hidaya,
Tanzania namba moja, kwa mpira wa mdomo!

No comments: