Monday, February 27, 2012

Waniua polepole

Laiti ungelijua, hapa nilipotulia,
Muziki nausikia, laini uliokuwa,
Maneno unayotia, moyoni yanaingia,
Waniua polepole, kwa wimbo unaouimba!


Naona yanielekea, kila nikiyachungua,
Nguo zangu yanivua, na uchi nikabakia,
Na wala sijakujua, nawe haujanijua,
Waniua polepole, kwa wimbo unaouimba!

Waimba kama wajua, kile ninachofikiria,
Mawazo wayachukua, yangu ninayowazia,
Kwenye wimbo ukatia, kama wanizungumzia,
Waniua polepole, kwa wimbo unaouimba!

Nabakia kushangaa, roho moja tumekua,
Na moyo wanipalia, na kwikwi kunikamia,
Natamani kujitoa, siwezi kujinyanyua,
Waniua polepole, kwa wimbo unaouimba!

Masahibu ya dunia, unayoyaelezea,
Yamefinika radhia laiti ungelijua,
Ninazidi kuumia, ninatamani kulia,
Waniua polepole, kwa wimbo unaouimba!

Laiti ungelijua, ungeleta kitambaa,
Machozi nikafutia, na kisha kukurejeshea,
Ungeujua ukiwa, moyoni uliokuwa,
Waniua polepole, kwa wimbo unaouimba!

Laiti ungelijua, mkono ungenigea,
Nipate kukuegemea, wakati ninatembea,
Nyumbani nikarejea, kwenda mwenyewe kulia,
Waniua polepole, kwa wimbo unaouimba!

Laiti ungelijua, wimbo ungelichagua,
Mwingine kujiimbia, kama huu usiokuwa,
Machozi nisingetoa, pasiwe pole kupewa,
Waniua polepole, kwa wimbo unaouimba!

No comments: