Wednesday, February 1, 2012

Ubinafsi wazimu

Hukua na ukakua, vigumu kuuzuia,
Akili waliokuwa, wakaja kuwa vichaa,
Kisha wakadhania, wengine ndio vichaa,
Ubinafsi hukuwa, ukawa nusu kichaa,
Huiba bila kujua!

Nguo watajazivua, hadharani walokuwa,
Kisha wakajidhania, majoho wameyavaa,
Ya dhahabu yalokuwa, na vito kunakshiwa,
Ubinafsi hukuwa, ukawa nusu kichaa,
Huiba bila kujua!

Yetu hawatasikia, mashindano hukua,
Kila mmoja akimbia, juu sana kuja kuwa,
Wengne kuwazidia, ubora akajaliwa,
Ubinafsi hukuwa, ukawa nusu kichaa,
Huiba bila kujua!

Neema huililia, hata haramu ikiwa,
Vya watu huvibugia, matumbo yazidi jaa,
Iwe kazi kupumua, wanavyojishindilia,
Ubinafsi hukuwa, ukawa nusu kichaa,
Huiba bila kujua!

Kila kitu hukitwaa, hata vya mbali vikiwa,
Na feha zikijaa, nje huzihamishia,
Na nyumba kuongezea, waishi wake bandia,
Ubinafsi hukuwa, ukawa nusu kichaa,
Huiba bila kujua!

Vigumu kuangalia, nchi wanachoingizia,
Wanajua kutumia, kuingiza ni balaa,
Kazi yao ni sanaa, kuunda hawajagundua,
Ubinafsi hukuwa, ukawa nusu kichaa,
Huiba bila kujua!

Wengine wakifa njaa, hujisunda kwa ridhaa,
Hupitisha na sheria, kuwalinda wakizoa,
Mwizi akavumiliwa, kiongozi kwendelea,
Ubinafsi hukuwa, ukawa nusu kichaa,
Huiba bila kujua!

Kweli huu ukichaa, hawajui wasojua,
Wapora wasiokuwa, cha kwao wakachukua,
Ukubwa kwao kuzoa, si wengine kuwafaa,
Ubinafsi hukuwa, ukawa nusu kichaa,
Huiba bila kujua!

Sisi tuliozoea, wa asili ujamaa,
Ukiritimba ukiwa, hakika twachanganyikiwa,
Kwa tusiowadhania, wanyama wote wakawa,
Ubinafsi hukuwa, ukawa nusu kichaa,
Huiba bila kujua!


Februari 1, 2012
Dar es Salaam

No comments: