Wednesday, February 1, 2012

Mvi taji la uzee

SI busara si hekima, mvi koja la uzee,
Kula aliye adhama, nafusi aifungue,
Ni muda wa kujituma, mema watu uachie,
Mvi taji la uzee, si busara si hekima!

Si muda wa kujinoma, wengine uwazuie,
Na madhambi kuchuma, kwa kutaka chako kiwe,
Na wengine kuwazima, upendacho wasitwae,
Mvi taji la uzee, si busara si hekima!

Wakati wa kuegema, ulozua uezue,
Ukapunguza hasama, na Mola umwagukie,
Ukitafuta rehema, si vigumu ugawiwe,
Mvi taji la uzee, si busara si hekima!

Ni wakati wa kusoma, usojua uyajue,
Kisha upange kalima, wengine uwaambie,
Kwa vitabu kujituma, tini uwachapishie,
Mvi taji la uzee, si busara si hekima!

Watambuao huzama, ya kesho waangalie,
Nalo hawatasimama, hadi tena wasipumue,
Mengineyo ni hujuma, yanaozesha uzee,
Mvi taji la uzee, si busara si hekima!

Tamaa huwa kilema, ikifikia uzee,
Huibuki utazama, bwawani utumbukie,
Ikawa huonekani, hata watu wazamie,
Mvi taji la uzee, si busara si hekima!

Husoma mwenye hekima, alama azitambue,
Wakati wenye uzima, ya kwake ajifanyie,
Na taa zinapozima, kitandani aingie,
Mvi taji la uzee, si busara si hekima!

Uzee si kulalama, maumivu yapungue,
Uzee kubwa heshima, ibadani ubakie,
Pumzi zako ghanima, kwa dua uongezee,
Mvi taji la uzee, si busara si hekima!

Februari 1, 2012
Dar es salaam.

No comments: