Wednesday, February 29, 2012

Shabiki si mzalendo

Michezo sio siasa, na siasa si mchezo,
Michezo budi hamasa, mikazo na mashikizo,
Na anasa kuzisusa, pamwe pasiwe mizozo,
Shabiki si mzalendo, mzalendo mshindani:
Asokubali kushindwa,
Kwa kuwa na kilichoundwa,
Wachezaji kuwezeshwa!

Michezo yataka panga, na wala si kupangua,
Michezo yataka anga, tanafusi na kutua,
Michezo yataka twanga, na wala si kutenguliwa,
Shabiki si mzalendo, mzalendo mshindani:
Asokubali kushindwa,
Kwa kuwa na kilichoundwa,
Wachezaji kuwezeshwa!

Ushindani kukimbia, sio kurudi nyuma,
Michezo budi hatua, kujua na kung'amua,
Moyoni wasiokuwa, hawawezi kutufaa:
Shabiki si mzalendo, mzalendo mshindani:
Asokubali kushindwa,
Kwa kuwa na kilichoundwa,
Wachezaji kuwezeshwa!

Michezo ni kukomaa, mazoezi na afya,
Chakula kinatakiwa, na vinywji kujinywea,
Mtiririko ukawa, katu usiopungua:
Shabiki si mzalendo, mzalendo mshindani:
Asokubali kushindwa,
Kwa kuwa na kilichoundwa,
Wachezaji kuwezeshwa!

Ushabiki Tanzania, njaa uliozidiwa,
Watu wanashabikia, vibovu vilivyokuwa,
Huku wamategemea, maajabu kutokea,
Shabiki si mzalendo, mzalendo mshindani:
Asokubali kushindwa,
Kwa kuwa na kilichoundwa,
Wachezaji kuwezeshwa!

Makocha wanatakiwa, hilo hatujakataa,
Na walimu waliokuwa, wajua saikoljia,
Na kisomo kugawia, watu wakajikomboa:
Shabiki si mzalendo, mzalendo mshindani:
Asokubali kushindwa,
Kwa kuwa na kilichoundwa,
Wachezaji kuwezeshwa!

Visiki tunavilea, ni lazima kujikwaa,
Viongozi wachaguliwa, mashaka wananitia,
Kama wanaganga njaa, au kuongoza wajua:
Shabiki si mzalendo, mzalendo mshindani:
Asokubali kushindwa,
Kwa kuwa na kilichoundwa,
Wachezaji kuwezeshwa!

Heri kujinyamazia, kwa macho kuangalia,
kama mbali twafikia, olympiki ikiwa,
Tayari nimeotea, watupu twajirudia:
Shabiki si mzalendo, mzalendo mshindani:
Asokubali kushindwa,
Kwa kuwa na kilichoundwa,
Wachezaji kuwezeshwa!

No comments: