Tuesday, February 28, 2012

Usijisifie kwa mema

VIUMBE wasio haya, si kazi kujisifia,
Ndio wasiojaliwa, hutaka kujinyanyua,
Hata kwa yasiyokuwa, watu hali wawajua,
Usijisifie mema, ukayavua mabaya
!


Kiumbe umelemewa, na wewe unayajua,
Vipi unayachukua, usoweza kuchukua,
Au haujatambua, kwamba ndefu sana yako njia,
Usijisifie mema, ukayavua mabaya!

Kiumbe wapungukiwa, halijajaa gunia,
Vipi unalitoboa, na begani kulitia,
Njiani halitoishia, nawe bila ya kujua?
Usijisifie mema, ukayavua mabaya!

Kiumbe waharibikiwa, wadhani wabarikiwa,
Hali ya hewa wachafua, wadani unaifagia,
Nahofu utapaliwa, ukweli ukijaujua,
Usijisifie mema, ukayavua mabaya!

Mema unajisifia, watu usowatendea,
Mazuri wajivalia, nje ukawavutia,
Hali ndani umejaa, uchafu wa kutitia,
Usijisifie mema, ukayavua mabaya!

Ya watu wachangamkia, yako yanakushushua,
Nje unapalilia, hali ndani hujasia,
Kila nikikuangalia, nashindwa kukuelewa,
Usijisifie mema, ukayavua mabaya!

Ndani nanga budi tia, ndiko kutakakokufaa,
Vinginevyo utapwaya, siku yakikutokea,
Yako usiposhikiliya, wengine ukaachia,
Usijisifie mema, ukayavua mabaya!

Wema ndani hutakiwa, kwako ukajiotea,
Kisha ukapalilia, na daima kuulea,
Nyuma yako hutulia, na Rabi kuwajalia,
Usijisifie mema, ukayavua mabaya!

Wema ukishautoa, soma njema yako dua,
Mlipaji ni mmoya, wa pili hajatokea,
Ahadi keshaitoa, mwongozo ukiangalia,
Usijisifie mema, ukayavua mabaya!

Punje ndogo azijua, na hesabu aitia,
Hapana cha kupotea, hulipwa kitu sawia,
Vingine haijakuwa, amini na zingatia,
Usijisifie mema, ukayavua mabaya!

No comments: