Monday, February 20, 2012

Wachimba shimo jipya ?

Sera za kujiumbua, ndizo unazotumia,
Wachimba shimo jipya, la zamani kufukia?
Hayo yataendelea, hapo hayataishia,
Wachimba shimo jipya, la zamani kufukia ?

Jifunze kujiparua, mkono unapofikia,
Zaidi ikizidia, utakuja umbuliwa,
Wafaa kisichofaa, kweli waharibikiwa,
Wachimba shimo jipya, la zamani kufukia ?

Maisha kukadiria, ndivyo inavyotakiwa,
Hatua kutozidia, uwezayo kuchukua,
Hakika mbaya tamaa, wengi sana imeua,
Wachimba shimo jipya, la zamani kufukia ?

Wachosha mwanaizaya, ya kwako kizaazaa,
Husikii ya kuambiwa, huonywi ukatulia,
Kisomo cha kuambaa, wataka tuharibia?
Wachimba shimo jipya, la zamani kufukia ?

Kaa ulikohamia, nasi kwetu tunakaa,
Usije kutulilia, nasi hatutakulilia,
Thamani umepungua, uzazi umebakia,
Wachimba shimo jipya, la zamani kufukia ?

Mbali sana tungekuwa, akili ungelijaliwa,
Wafanza tusoyajua, mwenyewe unayajua,
Na hatutaki kujua, yafiche yende kukuua,
Wachimba shimo jipya, la zamani kufukia ?

Kila mtu akushangaa, na sasa yajua dunia,
Hata nikijiondokea, mbaya watakujua,
Watoto nawaachia, ushahidi ulokuwa,
Wachimba shimo jipya, la zamani kufukia ?

Hadi mwisho wa dunia, ushahidi wabakia,
Ulivyokengeukiwa, na laana ilokuwa,
Mate waje kukutemea, mzazi usiyefaa,
Wachimba shimo jipya, la zamani kufukia ?

No comments: