Sunday, February 26, 2012

Binadamu si mashine

Hukuumbwa mashine, binadamu nakwambia,
Wapaswa kujitambua, akili kuitumia,
Watu wakikutumia, unakuwa ni kifaa,
Binadamu si mashine, apaswa kufikiria!

Itihari kajaliwa, kupima na kuchagua,
Afanye linalofaa, muktadha kuujua,
Na haki kuzingatia, kazini anapokuwa,
Binadamu si mashine, anapaswa kuchagua!

Ubongo kazawadiwa, apaswa kuutumia,
Na akishajipimia, mwenyewe akaamua,
Kwa vigezo vilokuwa, na watu na matukio,
Binadamu si mashine, anapaswa kuamua!

Vinginevyo ni bandia, mwanasesere akawa,
Wawe wamchezea, juu walotangulia,
Dhambi kumuachia, mwenyewe kujibebea,
Binadamu si mashine, apaswa kufikiria!

Wanasiasa balaa, fani yao yalaniwa,
Watu shere watezea, kama taahira wawa,
Ikawa wawakubalia, hata kwa yasiyokuwa,
Binadamu si mashine, anapaswa kuchagua!

Enzi zimeshaingia, watu kujiangalia,
Uhuru wakachagua, na haki kuzingatia,
Pasiwe wa kutumiwa, hadaa na kuzainiwa,
Binadamu si mashine, anapaswa kuamua!

No comments: