Monday, February 27, 2012

Waniua taratibu

Taratibu waniua, kila ukiniangalia,
Nyimbo unayoghania, moyoni yaniingia,
Kisha waangalia, kama moyoni watua,
Waniua taratibu, nami naona adha bu:
Kupenda ninaogopa!

Taratibu najifia, sithubutu kuzoea,
Kujaribu nakataa, na kuweza sijajua,
Ila nilichoshudia, mikono imeungua,
Waniua taratibu, nami naona adha bu:
Kupenda ninaogopa!

Sumaku yashabikia, vyuma inajivutia,
Miye ninashupalia, kuondoka haitokuwa,
Hapahapa ninakaa, hadi nguvu kukwishia,
Waniua taratibu, nami naona adha bu:
Kupenda ninaogopa!

Sitaki kukaribia, maafa ninayajua,
Heri mwanzo inapokuwa, mwisho huja kujutia,
Kila alojeruhiwa, hatari huzikimbia,
Waniua taratibu, nami naona adha bu:
Kupenda ninaogopa!

No comments: