Monday, February 20, 2012

Babu wetu Senegali

Ubabu aukataa, Ikulu kafurahia,
Pengine hawezi kaa, uzeeweye kuulea,
Miaka kajiongezea, kwa katiba kubomoa,
Babu wetu Senegali, vitukuu akimbia!

Babu wa demokrasia, sasa anaipindua,
Tamaa yamzidia, dhuluma kukumbatia,
Maamuzi kuamua, ya haki kuzifumua,
Babu wetu Senegali, vitukuu akimbia!

Mzee kajiachia, kwa fuli kujiachia,
Ukubwa amenogewa, adai kuongezewa,
Na watu sasa aua, malengo kuja timia,
Babu wetu Senegali, vitukuu akimbia!

Viongozi wenye njaa, Afrika watuumbua,
Umri wautania, pengine kwa kutumiwa,
Kitini kujasinzia, mambo huku yaamuliwa,
Babu wetu Senegali, vitukuu akimbia!

Sie tuliyemjua, vile alivyoanzia,
Watu kinyonga wakiwa, dunia huwashangaa,
Na kilichokuwa, dia, thamani kikatungua,
Babu wetu Senegali, vitukuu akimbia!

Ndour nakuruhumia, upotu unaotokea,
Nchi yashindwa kujua, vijiti pa kuachia,
Mbio zikaendelea, malengo yakafikiwa,
Babu wetu Senegali, vitukuu akimbia!

Watu wanapoachiwa, uungu hujiumbia,
Wakaja kuaminia, saa zote watakiwa,
Na wao isipokuwa, nchi haiwezi kuwa,
Babu wetu Senegali, vitukuu akimbia!

Ni ujinga uliojaa, Afrika waenea,
Yafaa kuwaondoa, nafasi wakaijua,
Ukiwa usipokuwa, nchi itaendelea,
Babu wetu Senegali, vitukuu akimbia!

Manani kutuangalia, lazima kusoma dua,
Yetu kutukubalia, na shida kuziondoa,
Yeye ni wa kubakia, wengine twajipitia,
Babu wetu Senegali, vitukuu akimbia!

Februari 20, 2012
Dar es Salaam. Tanzania.

No comments: