Thursday, February 23, 2012

Kila ukipanda juu

Ukubwa si juu kuwa, ila mengi kuachia,
Na kutofijiria, ila kuwafikiria,
Walokuwa raia, kiongozi kwao kuwa,
Kila ukipanda juu, yako yatakiwa yafe:
Ya wenzio uyajali!

Ukubwa kunyenyekea, na wala si kukemea,
Mtu hivyo akikua, uongozi humpwaya,
Ukubwa kutumikia, na sio kutumikiwa,
Kila ukipanda juu, yako yatakiwa yafe:
Ya wnanchi uyajali!

Ukubwa kuangalia, shida ukazitatua,
Sio kujinyamazia, mwenyewe ukajilia,
Hali hivyo ingekuwa, nchi zisingeendelea,
Kila ukipanda juu, yako yatakiwa yafe:
Ya raia uyajali!

Ukubwa nyumbani kukaa, si njiani kutembea,
Muda wa kufikiria, ni mchache ulokuwa,
Na kila kiguu na njia, adimu kuupatia,
Kila ukipanda juu, yako yatakiwa yafe:
Ya wenzio uyajali!

Ukubwa kusaidia, na sio kusaidiwa,
Watu ukanyanyua, nawe wakakunyanyua,
Ni rahisi wa kutoa, na mgumu kupokea,
Kila ukipanda juu, yako yatakiwa yafe:
Ya wnanchi uyajali!

Ukubwa kuangazia, fursa kuzitambua,
Jamii kuinyanyua, sio kwenda ikandia,
Nyuma asiyefatiwa, ukubwa humuumbua,
Kila ukipanda juu, yako yatakiwa yafe:
Ya raia uyajali!

Cheo kujitegemea, na sio kutegemea,
Ubunifu kuuzua, kwa mweyewe kuwazia,
Sio ndoto kuotea, mahala zisipofaa,
Kila ukipanda juu, yako yatakiwa yafe:
Ya wagonjwa uyajali!

Ukubwa kimya kukaa, na machache kuongea,
Na watu kujionea, mambo yanavyochanua,
Kubwabwaja historia, ni ujinga na hadaa,
Kila ukipanda juu, yako yatakiwa yafe:
Ya wajinga uyajali!

Ukubwa kuwatumia, watu wawe wakufaa,
Sio kuwasaidia, mizigo iliyokuwa,
Na walioendelea, hili wanalitambua,
Kila ukipanda juu, yako yatakiwa yafe:
Ya fukara uyajali!

No comments: