Wednesday, February 1, 2012

Huwachukia raia

RAIA huwachukia, ukweli wanaomwambia,
Kiongozi roho mbaya, haishi kuchanganyikiwa,
Na kila akiamua, mkenge hachi kwingia,
Huwachukia raia, kiongozi mnafiki!

Watu atawabagua, wema na wake wabaya,
Kama vile anajua, moyoni yaliyokuwa,
Umungu atajitia, kumbe shetani kamvaa,
Huwachukia raia, kiongozi mnafiki!

Uongo huusikia, kisha akazingatia,
Kila akikosolewa, vibaya hujisikia,
Badala kuongolewa, hatoacha kupotea,
Huwachukia raia, kiongozi mnafiki!

Nafsi humtangulia, roho ikafuatia,
Kujua akajitia, hata asiyoyajua,
Wenye hoja husinzia, nafasi wakamwachia,
Huwachukia raia, kiongozi mnafiki!

Ujibari hujitia, dhihaka kukomalia,
Mafuu humdhania, akili waliokuwa,
Ila watamuambaa, ahadiye kutimia,
Huwachukia raia, kiongozi mnafiki!

Kisasi hukusudia, ukubwa kuutetea,
Hujeruhi na kuua, akachezea dunia,
Na Mola humuachia, madhambi kumwongezea,
Huwachukia raia, kiongozi mnafiki!

Februari, 2012
Dar es Salaam

No comments: