Saturday, February 4, 2012

Kikombe nilichopewa

Kikombe kilivyokuwa, vyema kunakshiwa,
Mistari ilotiwa, dhahabu kumiminiwa,
Hakika nilidhania, miye nimebarikiwa,
Kumbe ni cha nuksi, kikombe nilichopewa!

Masikini sikujua, ni kikombe cha balaa,
Huko kilikotokea, kumbe kimeshalaniwa,
Na madhara kuchukua, miye nikayavamia,
Kumbe ni cha nuksi, kikombe nilichopewa!

Kizito kimeshakua, mkononi kunyanyua,
Kila nikiangalia, sina pa kukiachia,
Kikivunjika najua, mauti atanitwaa,
Kumbe ni cha nuksi, kikombe nilichopewa!

Sina wa kunipokea, ila nguo kujivua,
Uchi nipate bakia, jamiya kunishangaa,
Aibu naihofia, sithubutu kujivua,
Kumbe ni cha nuksi, kikombe nilichopewa!

Nalia mwana kujua, hiki nisingepokea,
Sumu kilishaingia, na ni vigumu kuitoa,
Kunywa ninaamriwa, na tone kutobakia,
Kumbe ni cha nuksi, kikombe nilichopewa!

Kumbe ni cha nuksi, kikombe nilichopewa!

Mashaka yanipopoa, moyo haujatulia,
Ninashindwa kuamua, wala pa kusogezea,
Kila nikijisumbua, macho watu wamekaa,
Kumbe ni cha nuksi, kikombe nilichopewa!

Kunywa ninasubiriwa, kutema sijaruhusiwa,
Na niliowateua, anguko langu najua,
Huruma inaniua, kubeba wasiokuwa,
Kumbe ni cha nuksi, kikombe nilichopewa!

Kikombe nilichopewa, siwezi kukikataa,
Napaswa kuvumilia, na dua sana kutoa,
Amebakia Alaa, kwa hili kuniokoa,
Kumbe ni cha nuksi, kikombe nilichopewa!

Februari 5, 2012,
Dar es Salaam.

No comments: