Monday, February 20, 2012

Uongozi mtihani

Kila anayeyajua, uongozi huchelea,
Mola testi atoa, kupima wanaojua,
Haki wakaitumia, na mema kulingania,
Uongozi mtihani, watakao hawajui!

Ila wasiyoyajua, mapema hukimbilia,
Wakidhania raha, na sifa itayokuwa,
Wakianza jaribiwa, uadui huuzua,
Uongozi mtihani, watakao hawajui!

Wapendwao huchukiwa, adui kutamaniwa,
Na nyoka ndani wakawa, watunzwa na kutulia,
Sumu huing'ang'ania, hata kuja kumuua,
Uongozi mtihani, watakao hawajui!

Ndivyo ilivyo dunia, urafiki haijawa,
Yapenda kuangalia, na watu kuwazomea,
Na wasioielewa, kudhani yafurahia,
Uongozi mtihani, watakao hawajui!

Wachache wanaingia, firdausi radhia,
Huanguka wakavia, na kuikata tamaa,
Mitihani huwafua, wakadha wakafuliwa,
Uongozi mtihani, watakao hawajui!

Wafuasi huwajia, madhambi wakaingia,
Na nyumbani nako pia, wake watamtumia,
Na wana wakachangia, maovu kutumbukia,
Uongozi mtihani, watakao hawajui!

Na siasa zenye njaa, waovu wakivamia,
Kila siku hesabia, dhambi za kimilionea,
Moto hautokimbia, ila ukijapendelewa,
Uongozi mtihani, watakao hawajui!

Maamuzi ukitoa, haki yaliyokimbia,
Nawe utahesabiwa, dhuluma umewafanyia,
Watu wakitoa dua, dhambi nawe kugawiwa,
Uongozi mtihani, watakao hawajui!

Israfu ikimea, nayo ngingine balaa,
Watu usipowaokoa, mikononi kukufia,
Utakuja hesabiwa, ndiye uliyewaua,
Uongozi mtihani, watakao hawajui!

No comments: