Monday, February 20, 2012

Utajafika wakati

Kila jambo linaanza, na kisha likaishilia,
Hawa waliyoyaanza, nayo yatamaliziwa,
Giza walilotutia, nalo likaondolewa,
Utajafika wakati, wezi watatokomea!

Wote wanotuibia, tamati itafikia,
Chini waende kukaa, machoni wakapotea,
Na mwisho ndipo huwa, wakaacha kuwajua,
Utajafika wakati, wezi watatokomea!

Kila ukitoa dua, Mola anaisikia,
Vingine kufikiria, mja waenda potea,
Hapo hapo shikilia, majibu kuyangojea,
Utajafika wakati, wezi watatokomea!

Mengi watajifanyia, kwa haki kuzinunua,
Vyote ataporomoa, mkuu aliyekuwa,
Siku akizimia, kwa dua kuwasikia,
Utajafika wakati, wezi watatokomea!

Usipoyashuhudia, mwanao atajionea,
Wakati ukifikia, hakuna wa kuzuia,
Ndivyo inavyokuwa, toka dunia kutua,
Utajafika wakati, wezi watatokomea!

Wasiwasi kutokuwa, majibu hayatapotea,
Dakika inangojewa, saa iliyopangiwa,
Huyu mwenye kutimia, hakuna asilojua,
Utajafika wakati, wezi watatokomea!

Hurithi wasiokuwa, kizazi kujimegea,
Kwa ajabu zake njia, wewe wabaki shangaa,
Ndivyo ilivyo dunia, na hizo ni zake njia,
Utajafika wakati, wezi watatokomea!

Si kila kinacholiwa, tumboni kitaingia,
Ardhini huishia, kingi kinachozaliwa,
Na ndivyo inavyokuwa, ajabu yake dunia,
Utajafika wakati, wezi watatokomea!

Sio tu kwa raia, hadi na waheshimiwa,
Gaddafy ungemjua, huachi msikitikia,
Kila alichoambulia, sasa mchanga keshakuwa,
Utajafika wakati, wezi watatokomea!

Na wengine walokuwa, leo wameshafukiwa,
Waliitaka dunia, lakini imewakataa,
Yenyewe inabakia, hakuna wa kubakia,
Utajafika wakati, wezi watatokomea!

No comments: