Sunday, February 5, 2012

Mja kaumbwa na haraka

Kazi ya mtu kama pia, ni kukimbiakimbia,
Hawezi akatulia, la msingi kulizua,
Na yake ni kutumia, wala si kutwingizia,
Mja kaumbwa na haraka, kwa yake sio ya Mola!

Haraka ameumbiwa, bila mwisho kuujua,
Ila ibada huzua, sababu kadha wa kadhaa,
Ndivyo inavyotokea, hadi kuaga dunia,
Mja kaumbwa na haraka, kwa yake sio ya Mola!

Hatukuumbwa tambua, kwa jingine manufaa,
Ila ibada na dua, ishirini na nne dia,
Saba kwa juma jamaa, mengine yakafatia,
Mja kaumbwa na haraka, kwa yake sio ya Mola!

Haya ukiyaachia, shetani utamvaa,
Kisha akakuhadaa, kwa wengine kupitia,
Ukija kushtukia, umekwishaangamia,
Mja kaumbwa na haraka, kwa yake sio ya Mola!

Mola kumgeukia, ni wakati wa kufaa,
Toba kushughulikia, na mingine misamaha,
Kamwe hautochelewa, kwa Muumba kurejea,
Mja kaumbwa na haraka, kwa yake sio ya Mola!

Februari 6, 2012,
Dar es Salaam.

No comments: