Thursday, February 2, 2012

Nchi inayodhulumu maskini

Ni sinema wanakuwa, ya Chalii Chaplini,
Kazi ni kujishushua, wawe kwenye skrini,
Hilo yore yanavia, hawana lenye thamani,
Nchi inayodhulumu, raiawe masikini,
Wakubwa hulaaniwa, wakakosa mengi sana,
Na kubwa na la kutisha,
ni kukosa hata chembe,
ya hekima na busara!

Wazee wastaafu, na hali ni masikini,
Wanazo zake sharafu, muogopewa Manani,
Nyoyo zikiwa si kufu, ustawi mashakani,
Nchi inayodhulumu, raiawe masikini,
Wakubwa hulaaniwa, wakakosa mengi sana,
Na kubwa na la kutisha,
ni kukosa hata chembe,
ya hekima na busara!

Wajane wanaoibiwa, na walo madarakani,
Dola na wanasheria, dhulumati wasihini,
Jalali hatoridhia, watu hutia shakani,
Nchi inayodhulumu, raiawe masikini,
Wakubwa hulaaniwa, wakakosa mengi sana,
Na kubwa na la kutisha,
ni kukosa hata chembe,
ya hekima na busara!

Huduma wasipopewa, walioko vijijini,
Ikawa kusahauliwa, yao siyo hesabuni,
Mioyo ikiumia, nchi huwa taabani,
Nchi inayodhulumu, raiawe masikini,
Wakubwa hulaaniwa, wakakosa mengi sana,
Na kubwa na la kutisha,
ni kukosa hata chembe,
ya hekima na busara!

Wakubwa wataugua, na kwishia ajalini,
Maofisi kuungua, na mafuriko kughani,
Pepo hazitatulia, kwenye kona zote nchini,
Nchi inayodhulumu, raiawe masikini,
Wakubwa hulaaniwa, wakakosa mengi sana,
Na kubwa na la kutisha,
ni kukosa hata chembe,
ya hekima na busara!

Nalilia Tanzania, eti nchi ya amani,
Wanyonge wanaumia, tena hawana thamani,
Na wakubwa wanajua, ila nao majinuni,
Nchi inayodhulumu, raiawe masikini,
Wakubwa hulaaniwa, wakakosa mengi sana,
Na kubwa na la kutisha,
ni kukosa hata chembe,
ya hekima na busara!

No comments: