Sunday, February 26, 2012

Watu wao wapigao

Ni wale tuwajuao, nao ni kawaida yao,
Ukubwa wautakao, wale wao na wakwao,
Walinzi wafugwao, kulinda wakubwa wao,
Watu wao wapigao, si amani watakao!

Hudhani wao ni wao, na nchi hii ni yao,
Katiba wapinduao, juu kujiweka wao,
Na wananchi walalao, wakawa nalo pumbao,
Watu wao wapigao, si amani watakao!

Wasijue kuwa wao, ndio wao wafukuzao,
Asibaki mmojawao, zahama ikija kwao,
Uwe ni mwisho wao, na mwanzo wa wajuao,
Watu wao wapigao, si amani watakao!

Sauti ni nyie mnayo, na mambo muamuoa,
Mkitaka watoke wao, kutoka lazima kwao,
Isiwe ni warudio, juu tena sio yao,
Watu wao wapigao, si amani watakao!

Ni nyie muwawekao, na muamalizao,
Kwa lenu moja amuo, watoke hapo si kwao,
Wako wengi wenzao, nafasi waitakayo,
Watu wao wapigao, si amani watakao!

Haitoshi wajivuao, gamba liozalo kwao,
Na ngozi yenye kumbao, mwilini wabakiayo,
Uchago hulia wao, waulaliapo mwao,
Watu wao wapigao, si amani watakao!

Naamba niwaambiao, nyakati hizi si zao,
Mabadiliko ni ngao, huvunjika zao tao,
Yajayo si wazuiayo, watatoka watokao,
Watu wao wapigao, si amani watakao!

Kivumbasi mwanakwao, heri si wajaliwao,
Shetani ana kikao, mara kwa mara nao,
Na haya waamuayo, mwayaona yazuayo,
Watu wao wapigao, si amani watakao!

Urithi si watakao, wawapa kwanza wanao,
Kuua ni jadi yao, na wala sio wazaao,
Mti hujazaa mbao, si mbao yenye uzao,
Watu wao wapigao, si amani watakao!

No comments: