Thursday, February 23, 2012

Za sitini na sabini

Miye nilijiamini, katika hii dunia,
Nilizilishwa hisani, hadi moyo kujaa,
Sikuwa ni msshakani, kila nilipoingia,
Nazikumbuka mwenzenu, za sitini na sabini.

Ninakumbuka shambani, na niliyojisomea,
Mimea kuithamini, na viumbe kuwalea,
Najiona majinuni, watoto wasivyojua,
Nazikumbuka mwenzenu, za sitini na sabini.

Nakumbuka ya nyumbani, na ugenini pia,
Muziki wenye anwani, moyoni uloingia,
Na maudhui ya undani, kitu uliyochukua,
Nazikumbuka mwenzenu, za sitini na sabini.

Nakumbuka vya thamani, vitu vilivyokikaa,
Si vitu kama utani, havikai huchakaa,
Na nyinginezo samani, hata zile za kubembea,
Nazikumbuka mwenzenu, za sitini na sabini.

Nakumbuka wanandani, walionikimbilia,
Nikawapoza ubani, na udi kuwapatia,
Na walonipa hisani, hadi hapa kufikia,
Nazikumbuka mwenzenu, za sitini na sabini.

Walimu wenye mizani, msingi wliokuwa,
Na sekondari mjini, Mawenzi walopitia,
Moshi na Mbeya mjini, na nilikotumikia,
Nazikumbuka mwenzenu, za sitini na sabini.

Maelezo wahisani, mdogo walinichukua,
Kazi kunipa mezani, uandishi kufatia,
Na kutumwa mikoani, habari kuwaletea,
Nawajua njendani, miaka niliyopitia,
Nazikumbuka mwenzenu, za sitini na sabini.

Ninakumbuka chuoni, na wapenzi walokuwa,
Tulipozila amini, kutoa sio kutwaa,
Na leo sina imani, wengine wamejifia,
Nazikumbuka mwenzenu, za sitini na sabini.

Wanafunzi duniani, wapo wanaonijua,
Niliwafunza imani, na akili kutumia,
Wakaacha ya kughani, mengi wakayafikiria,
Nazikumbuka mwenzenu, za sitini na sabini.

Nakumbuka ugenini, nje nilikosomea,
Ubelgiji yamini, Luveni iliyokuwa,
Masta nikaichukua, na pendo kuwaachia,
Nazikumbuka mwenzenu, za sitini na sabini.

Kufikia themanini, nilikuwa nimerejea,
Nimeishi ugenini, moyoni nyumbani ukiwa,
Ila sasa mtihani, mengine nayafikiria,
Nazikumbuka mwenzenu, za sitini na sabini.

Nakumbuka kwa yakini, nyimbo zilozotulia,
Zikikumbusha zamani, enzi zilizopotea,
Yamebaki maruhani, kichwani yakitembea,
Nazikumbuka mwenzenu, za sitini na sabini.

Sina lililo thamani, vyote vinshapotea,
Nimebaki upwekeni, wapenzi wamepotea,
Uzeeni siamini, afueni kutokea,
Nazikumbuka mwenzenu, za sitini na sabini.

No comments: