Friday, February 3, 2012

Baba



Mwana waweza mficha baba

Uwe mke wa ndoa au kahaba

Kijana akibalehe, aijue janaba

Mwali kivunja ungo bila ngariba

Huuliza baba, Huulizwa baba

Namtaka baba, Twamtaka baba

Ikawa adhaba, Japo wala na kushiba

Mzigo kubeba, ukamlilia naye wako toba

kuiepa shuruba, ili waache mama kukukaba

Ukajua nasaba, imejaa yake mahaba

Huwezi ukawa baba, mama wa mengi mahaba

Maana baba ni baba, nawe ni wake swahiba

Sio suala la haiba, hili ni la watu nasaba

Huwezi pengo kuziba, hata uzidishe mahaba

Utaifanya ghiliba, watoto wakakukaba

Hukuona wewe juba, nafusi yao unaiziba

Wakutafutie kiroba, ndani iwe ni yako ghuba

Na ya kwangu kwenu tiba, kutoitupa nasaba

Mbwani kiumbe hushiba, na mengine matlaba,

Haya kwao kama shaba, dhahabu kwao nasaba

Nasaba kwao mahaba, na chachandu ndiye baba!

Februari 4, 2012

Dar es Salaam.

No comments: