Wednesday, February 1, 2012

Waacha maji baridi

Bahati wasiopewa, hupata kikapotea,
Yalo mema huitiwa, nao wakayakimbia,
Pepo hutengenezewa, moto wakauchagua,
Waacha maji baridi, wakachota ya bahari!

Asali huiambaa, shubiri wakachagua,
Neema huikemea, balaa wakaridhia,
Nusura huikimbia, maasi wakaingia,
Waacha maji baridi, wakachota ya bahari!

Chumvi huichagua, sukari ikitakiwa,
Maji huyazidishia, ukavu unapotakiwa,
Gia ya nyuma hutia, ya mbele ikitakiwa,
Waacha maji baridi, wakachota ya bahari!

Chini hujifukia, juu wanapotakiwa,
Gizani hukomelea, nuru nje imejaa,
Milioni hutumia, wakati yatosha mia,
Waacha maji baridi, wakachota ya bahari!

Uoni huwapungua, uongo ukiwavaa,
Ya kweli huyakataa, uzaini kuridhia,
Juto mjukuu huwa, Joti wakamuachia,
Waacha maji baridi, wakachota ya bahari!

Februari 1, 2012
Dar es Salaam

No comments: