Saturday, February 18, 2012

Faida za Uranium

Busara imeambaa, ukubwa wameshalewa,
Haiwi haitokuwa, kwa wakati tulokuwa,
Faida nyingine kuwa, madini kuyachimbua,
FAIDA ya uranium, kwa Tanzania mauti!

Dini anayeijua, uongo ataambaa,
Au yakijafikia, mapari kutwambia,
Uranium inafaa, sasa kwendakuichimbua,
FAIDA ya uranium, kwa Tanzania mauti!

Masheikh wakafatia, na tiki kwenda itia,
Na hawa huru kuwa, na sio wanaotumiwa,
Hakika tunawajua, ukweli wanaojua,
FAIDA ya uranium, kwa Tanzania mauti!

Hautatusaidia, maneno kuharishia,
Yatosha tunayojua, vingine haitakuwa,
Uwekezaji balaa, twaona unanukia,
FAIDA ya uranium, kwa Tanzania mauti!

Cha mbele kinshatembea, hakuna cha kurejea,
Maisha yamepungua, thamani hayatakuwa,
Na wanaoyachochea, hakuna asiyewajua,
FAIDA ya uranium, kwa Tanzania mauti!

Chama kilicho na njaa, wanyonge chawahadaa,
Utu wasioujua, watu wema wajitia,
Afueni isokuwa, ndiyo inatarajiwa,
FAIDA ya uranium, kwa Tanzania mauti!

Wakati ninakataa, bado haujafikia,
Nusura haitakuwa, makaburi twachimbua,
Toka wanapoyatoa, hadi kwenda kuondoa,
FAIDA ya uranium, kwa Tanzania mauti!

Kisha twaenda changia, binadamu kuua,
Kwa pesa kujipatia, damu zilizomwagiwa,
Mola tunaamriwa, twapasa kweli kumjua,
FAIDA ya uranium, kwa Tanzania mauti!

Heri litakalokuwa, mimi sintolikataa,
Na njaa ninaijua, ni mzazi wa tamaa,
Huweza ukakimbilia, liendalo kukuua,
FAIDA ya uranium, kwa Tanzania mauti!

Nchi yangu ninalia, hatua uloingia,
NI kama umepagawa, na fikra kuepuliwa,
Tafakuri yalemaa, kama uliyechezewa,
FAIDA ya uranium, kwa Tanzania mauti!

Namkabidhi Jalia, pekee alobakia,
Watu wangu kuwajua, na kisha kuwaangalia,
Baya kuwaepushian na wabaya kuumbua,
FAIDA ya uranium, kwa Tanzania mauti!

No comments: