Kawarehemu Rabuka, waja wamebahatika,
Utawala katuvika, juu ya punda na nyoka,
Tokea hiyo miaka, Adamu alipomweka,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Kawafunza mamlaka, kutoa na kuiweka,
Nguvu umma kautwika, si mtu mmoja kubweka,
Naye analolitaka, ndilo linalofanyika,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Haki zote yazishika, hawezi mtu kupoka,
Mabavu anayetaka,kutumia hatofika,
Umma humpiga mweleka, pembeni akaanguka,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Wajinga wakishtuka, uongo kugundulika,
Hasira huwachemka, haki waanze kusaka,
Hapo huwa patashika, nchi iache kalika,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Ya wananchi mamlaka, ukuu unayashika,
Yenyewe inapotaka, mabadiliko kuzuka,
Hakuna kuzuilika, hata mabomu yakifoka,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Ukweli watu wataka, wachoka kudanganyika,
Haki zao kuzishika, maamuzi kufanyika,
Ni kosa kuhadaika, adhabu itawatoka,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Viongozi wastahika, wakiwa nayo hakika,
Kauli kutopotoka, au dhuluma kusuka,
Watafufuka mizuka, na misukule kuzikwa,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Ni kosa lilo dhihaka, kwa yeyote kupituka,
Hapatakuwa mwafaka, ustawi kukauka,
Hakuna kueleweka, wala atayeridhika,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Mchezo wa panya na paka, uanze vuka mpaka,
Wapandao wakashuka, walo tuli wakafoka,
Ije kuzuka gharika, wasiomo kuzoleka,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Mamlaka ikichoka, umma utataabika,
Mabavu ikiyapika, umma yakaufunika,
Wakafanzwa mateka, wasio na madaraka,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Katiba yahesabika, raia wanaishika,
Na kutoa na kuweka, ni ya kwao mamlaka,
Vingine ikifanyika, wizi wa kuaminika
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Sheria ikienzika, si wakubwa kujitwika,
Wasiopewa baraka, juu yetu mamlaka,
Nchi itavurugika, pasiwe pa kukalika,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Uchama sasa wahaka, wengi wanaodhurika,
Ni kufa na kufufuka, yanakithiri mashaka,
Wengine wanayataka, vyama kutokumeguka,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Ila taifa hakika, budi vyama kufunika,
Chama kufa ni hakika, taifa halitaanguka,
Taifa hubadilika, haitasambaratika,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Viongozi watatoka, wengine kujawaweka,
Mizizi kutingishika, nchi haitosumbuka,
Hapa mbali tumefika, hili lina uhakika,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Waoga wanatishika, nchi kusambaratika,
Ila wanachokitaka, bahati kikiishika,
Hii naona dhihaka, tena mkubwa mzuka,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Macho wameshafunguka, waliokidanganyika,
Wajanja wamewabaka, na mbinu zao kuteka,
Mambo yanaeleweka, hakuna lisilojibika,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Nasaha tunaeleka, waibao mamlaka,
Chini lazima kushuka, balaa kuepukika,
Vizazi kuhamanika, amani ikatoweka,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Nafsi juu kuweka, yalanika Afrika,
Ndiyo mnayotaka, Tanzania kuja zuka?
Waogopeni mahoka, wasije wakanyanyuka,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Ninamuomba Rabuka, viongozi kuwadaka,
Utovu ukawatoka, na tamaa kuwashika,
Sote tukasalimika, na mitihani kuvuka,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Tuacheni kuzuzuka, kwa vyeo tunavyoshika,
Tuwapeni madaraka, wananchi wastahika,
Maamuzi kufanyika, huria tunayotaka,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Upande kuegemeka, kwingine nani kushika,
Nchi itagawanyika, katu hatutaeleweka,
Wengine wakatucheka, muamana kuanguka,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Amkeni mloshika, Tanzania mamlaka,
Uzalendo kuusaka, mitihani kuivuka,
Katiba tunayotaka, isiwe ni ya mashaka,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Yarejeshwe mamlaka, wananchi kujayashika,
Maamuzi kufanyika, yasokuwa na wahaka,
Ya kwao wanayoyataka, wajue kwapambazuka,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Kung'ang'ana waloshika, hivi leo madaraka,
Kiwewe kimewashika, mchana waweweseka,
Kombe wataka funika, mwanaharamu kuvuka?
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
Siri gani yafichika, hadi wajinga wang'aaka.
Ni mifupa mlopachika, kabatini yemegeka?
Kwetu hakijaeleweka, ukweli tunautaka,
Uwizi wa mamlaka, mama wa yote madhambi!
© 2011 Sammy Makilla
Sunday, January 1, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment