Tuesday, December 13, 2011

China ni rafiki yetu

Mao sote twamjua, na Uchina kuikomboa,
Shule tulijisomea, na vyuoni kuandikia,
Tukabuni Ujamaa, Nyerere katuachia,
China ni rafiki yetu, twapaswa mshikilia!

Miaka mingi twajua, Nyerere katembelea,
Uchina akashangaa, kujituma ilivyokua,
Kaja akatuambia, udugu wanatufaa,
China ni rafiki yetu, twapaswa kufurahia!

Na sote tunatambua, China ilivyotufaa,
Chou-en-lai tambua, na Nyerere walianzia,
Ushirikiano ukawa, mwingi wenye manufaa,
China ni rafiki yetu, twapaswa mshikilia!

Wengine twakimbilia, kunyonya waliozoea,
Nchi wanainunua, na sisi tunasinyaa,
Viongozi twawajua, walio na manufaa,
China ni rafiki yetu, twapaswa mng'ang'ania!

Mzungu kumshabikia, anayetoka Ulaya,
Mmarekani naye pia, kazidi kuwazuzua,
Hawana wanachotufaa, ili kupe wamekua,
China ni rafiki yetu, twapaswa mzawadia!

Mchina katujengea, TAZARA walokataa,
Viwanda katuundia, wenyewe tumeviua,
Viwanja tunavijua, kwa jinsi vinavyong'aa,
China ni rafiki yetu, twapaswa mkumbatia!

Migodi angechukua, bure tusingeibiwa,
Vijiji vingelikua, hata wetu Ujamaa,
Wanafiki wajitia, ni sisi twaukataa,
China ni rafiki yetu, twapaswa mshikilia!

Treni wangechua, ni ya mbio ingekuwa,
Umeme kutumia, ndege wawili kuuua,
Kigoma ungeingia, si kwa siku ni masaa,
China ni rafiki yetu, twapaswa mpendelea!

Ndege tungechangia, ATC ingelikua,
Za kwao wajiundia, na wengine kununua,
Biashara waijua, na sisi tuna abiria,
China ni rafiki yetu, twapaswa kumsikia!

Mashamba tungemwachia, mapinduzi angezua,
Njaa ingelikimbia, na biashara ingekuwa,
Nje tungejiuzia, tukazidi endelea,
China ni rafiki yetu, twapaswa kumridhia!

Mashariki kwangalia, wito umeshatolewa,
Machweo yanaingia, Magharibi tunajua,
Kadri tunavyozubaa, wengi watatuondoa,
China ni rafiki yetu, twapaswa kulitambua!

Urafiki nautakia, uzidi kuendelea,
Uchina na Tanzania, hadi udugu ukawa,
Wabaya kuwakimbia, amani kuendelea,
China ni rafiki yetu, twapaswa mkumbatia!

No comments: