Thursday, December 1, 2011

Pendo lenye ubaridi

Ninashindwa kunyanyua, mikono yangu radhia,
Kifua kukuachia, uje kunikumbatia,
Pendo lako limepoa, halitanisisimua,
Pendo lenye ubaridi, kitanda hakilaliki!

Baridi lililokua, pendo huwa linavia,
Ni shida kuitikiwa, sembuse kukubaliwa,
Mkeka juu ulokua, hauwezi kukaliwa,
Pendo lenye ubaridi, kitanda hakilaliki!

Na chai iliyopoa, ni nani atajinywia,
Ladha huwa yapotea, na kama maji ikawa,
Motowe ukipotea, kahawa haitanywewa,
Pendo lenye ubaridi, kitanda hakilaliki!

Hili ni jambo la nasaha, wakati wote kujua,
Hata malau yakiwa, pendo lataka murua,
Kusahau yatakiwa, na mwenzi kumkubalia,
Pendo lenye ubaridi, kitanda hakilaliki!

Kamwe si yake tabia, pendo lililofubaa,
Wachache hulichukua, njaa ikiwazidia,
Ila wengi walokua, kabisa hulikataa,
Pendo lenye ubaridi, kitanda hakilaliki!

Frijini ukitia, mapenzi hujiozea,
Si chakula na bidhaa, muda mrefu kukaa,
Watakiwa kuelewa, usije kupotelewa,
Pendo lenye ubaridi, kitanda hakilaliki!

Pendo ni kuitikia, na si kugugumia,
Lataka kushikiliwa, wala sio kuachiwa,
Pendo ni kukumbatiwa, na sio kugeukiwa,
Pendo lenye ubaridi, kitanda hakilaliki!

Mikono naikunjua, nawewe moyo kunjua,
Kifuani kutulia, mapigo sawa yakawa,
Vidole vikitambaa, daima vinakojua,
Pendo lenye ubaridi, kitanda hakilaliki!

No comments: