Tuesday, December 13, 2011

Ndani ukishamuweka

Huenda akatulia, ndani ukishamuweka,
Yake kumtimizia, akawa anatosheka,
Tena hatojisumbua, kizingiti utaweka,
Ndani ukishamuweka, roho yako hutulia.

Nje ukimuachia, hutoipata hakika,
Yake hutoyajua, utazidi kubomoka,
Yako watayafichua, kote yakatangazika,
Ndani ukishamuweka, roho yako hutulia.

Mwenzangu sijakujua, kisa cha kuweweska,
Washindwa kufikiria, yale yanayoepukika,
Wewe unang'ang'ania, ukale kuusimika,
Ndani ukishamuweka, roho yako hutulia.

Tabia yakuumbua, huwezi kuaminika,
Kizazi kipya chajua, huko nyuma mlikotoka,
Wazazi wamehadaiwa, hawana waliloshika,
Ndani ukishamuweka, roho yako hutulia.


Wao wameshaamua, maisha wanayataka,
Leo leo wakwambia,hakuna kungojeleka,
Na usipowasikia, kazi yao itafanyika,
Ndani ukishamuweka, roho yako hutulia.

Ukizidi kushangaa, kote watakusanyika,
Mabango kuyainua, na watu wapya kutaka,
Nchi wakaishukua, wapate kusalimika,
Ndani ukishamuweka, roho yako hutulia.

Wimbo sijakuimbia, mbaya kuweweseka,
Ushauri nakugeea, uchukue ukitaka,
Dharau ukiamua, yawe yako kukufika,
Ndani ukishamuweka, roho yako hutulia.

Kazi yangu kutimia, kilingeni nakusaka,
Ya mjini kuyajua, cha leo kueleweka,
Nyumbani hakujatulia, njaa imeshafumuka,
Ndani ukishamuweka, roho yako hutulia.

No comments: