Thursday, December 1, 2011

Pendo lenye maumivu

Huzidisha uchakavu, pendo lenye maumivu,
Maisha huwa mabovu,na adimu usikivu,
Wenza hujaa makovu,rohoni na kwenye mbavu,
Pendo lenye maumivu, linahitaji wokovu!

Ni upendo tepetevu, uzidishao uchovu,
Yakithiri maumivu, mwilini kukosa nguvu,
Hunyauka hata ndevu, kiaktoweka kidevu,
Pendo lenye maumivu, linahitaji wokovu!

Ni hadithi ya mabavu, misuli pia maguvu,
Halinao uangavu, daima huwa ni kavu,
Latisha kama mafuvu, ukivua kwenye nyavu,
Pendo lenye maumivu, linahitaji wokovu!

Mkaa wake utovu, huishia kwenye jivu,
Wawili huwa wadhoofu, wembamba wao wa mavu,
Hujifanya ni werevu, kumbe wote ni waovu,
Pendo lenye maumivu, linahitaji wokovu!

Pendo hugeuka povu, kama sabuni angavu,
Kiwaungacho kitovu, hukatika kama nyavu,
Wote wakawa wavivu, kufufua yao 'lavu'.
Pendo lenye maumivu, linahitaji wokovu!

No comments: