Yunani asojijua, kabila humkataa,
Chasaka huwambiwa, nasaba ikapoea,
Kihamba hatogawiwa, ila kwa kupendelewa,
Asiyejua yunani, huiga yao wageni!
Mjini wameingia, wengi wasojijua,
Mambo waparamia, hata yasiyowafaa,
Huishia kupotea, wengine kuangamia,
Asiyejua yunani, huiga yao wageni!
Vijana wanaokua, mataa huwazuzua,
Wakaiga ya halua, tende wakaidhania,
Rangi huzichanganyia, usijue kilichokua,
Asiyejua yunani, huiga yao wageni!
Kwao walikotokea, ni nani hawakujua,
Na mjini wakiingia, wapya wajidhania,
Watayafuatilia, hata ya walaaniwa,
Asiyejua yunani, huiga yao wageni!
Kama mtoto ukiwa, kuiga huwa ni sawa,
Utu uzima kingia, watakiwa kujijua,
Kiumbe uliyekua, na ya kwako majaliwa,
Asiyejua yunani, huiga yao wageni!
Mola hakudhamiria, wote tukawa sawia,
KIla mtu kajaliwa, tofauti yeye kua,
Na anachotakiwa, kipaji chake kulea,
Asiyejua yunani, huiga yao wageni!
NI manyani walokua, kuiga wasiowajua,
Wengine maharamia, na watumwa walikua,
Utadhani ni vichaa, tabia wanazozua,
Asiyejua yunani, huiga yao wageni!
Mtoto unapotea, bado haujajijua,
Nafsi unatakiwa, sasa kuichungua,
Upate kujitambua, na kile utachokua,
Asiyejua yunani, huiga yao wageni!
Thursday, December 1, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment