Sura ya plastiki, wengi inawahadaa,
Kama taa za trafiki, njiani inavyong'aa
Ukiishika kaniki, haikawii kuchakaa,
Yang'ara kumbe uoza, sura ya plastiki!
Itazame halaiki, hili utaligundua,
Wengi wao wanafiki, nailoni wamevaa,
Kweli hawatambuliki, ila tunawadhania,
Yang'ara kumbe uoza, sura ya plastiki!
Kustahimili mikiki, hawawezi nakwambia,
Taabu hawaitaki, wanataka kulelewa,
Ila ni kama samaki, majini ukiwatoa,
Yang'ara kumbe uoza, sura ya plastiki!
Nakukanya Mwanabaki, plastiki kataa,
Usiilee ashiki, hata bure ukipwa,
Ngozi unayomiliki, hupendeza asilia,
Yang'ara kumbe uoza, sura ya plastiki!
Waache wanaotaliki, rangi waliyojaliwa,
Uzungu wakaulaki, na madawa kutumia,
Mwisho wakihamaki, hawana kilichobakia,
Yang'ara kumbe uoza, sura ya plastiki!
Asili wako rafiki, ya kuiga ni adawa,
Vinginevyo mushiriki, utajaadhibiwa,
Ringa na yako kaniki, mwana uliyojaliwa,
Yang'ara kumbe uoza, sura ya plastiki!
Ringa na yako kaniki, mwana uliyojaliwa,
Usitamani mamluki, ndani mwenu haitakaa,
Ukitaka ushabiki, ni ngozi yako kulea,
Yang'ara kumbe uoza, sura ya plastiki!
Thursday, December 1, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment