Dunia imepagawa, viumbe waichezea,
Vioja hali ya hewa, kila mtu ashangaa,
Kwa vuli zake mvua, masika zinaagua,
Vuli ikiwa masika, mkwezi huhamanika.
Vuli ilipotea, sasa imesharejea,
Hatukujiandaa, kwani hatukutegemea,
Sasa kinachotokea, miujiza imekua,
Vuli ikiwa masika, mkwezi huhamanika.
Kama vuli imekua, ndiyo masika yamwaa,
Ikija tunayojua, hali vipi itakua,
Hata nami nahofia, gharika kuja tokea,
Vuli ikiwa masika, mkwezi huhamanika.
Hii ni hali tabia, au tabia ya udhia,
Nani hali kahadaa, hadi zimechanganyikiwa,
Nini yake manufaa, au hasara itakuwa?
Vuli ikiwa masika, mkwezi huhamanika.
Tumeumbua dunia, au inatuumbua,
Masikio twafungua, na haya tumesikia,
Siku yakijaingia, vipi tutayakimbia?
Vuli ikiwa masika, mkwezi huhamanika.
Neema inapotea, maafa yanaingia,
Baa la kujitakia, wachache huja kulia,
Upweke utauvaa, na usononi kunawa,
Vuli ikiwa masika, mkwezi huhamanika.
Thursday, December 1, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment