Thursday, December 1, 2011

Hayawani

Hayawani afkani, na mkubwa majinuni,
Ameikosa imani, na sio mtu wa dini,
Hazitambui kanuni, ila ya kwake thamani,
Hayawani na miwani, bado wamwona usoni!

Hata akiwa ni nani, hayawani, hayawani,
Utampa cheo gani, uweze kumuamini,
Ndugu huwa hathamini, watu baki kitu gani,
Hayawani na miwani, bado wamwona usoni!

Ahadi hana mdomoni, kupayuka ni kanuni,
Tabia yake ni duni, huwezi kumuamini,
Vitendo vyake baini, vyaongozwa na shetani,
Hayawani na miwani, bado wamwona usoni!

Muelewe hayawani, ndugu yake mumiani,
Hukuuza maporini, msamaria udhani,
Ni viumbe wahaini, wadhani wana thamani,
Hayawani na miwani, bado wamwona usoni!

No comments: