Thursday, December 1, 2011

Usilazimishe jambo!

Jambo kutoharakia, ushauri wa kufaa,
Kitu ukikimbilia, madhara huja tokea,
Nenda kwa yako hatua, huwa litakalokua,
Usilazimishe jambo, likichelewa liache.

Subira kitu radhia, mitume watuambia,
Kila unalokusudia, si lazima kujaliwa,
Kaa kama usiyekaa, lijalo kuchangamkia,
Usilazimishe jambo, likichelewa liache.

Kwa taratibu tembea, kilomita hutimia,
Ukitaka endelea, waweza kudidimia,
Juu ukiazimia, chini utachukuliwa,
Usilazimishe jambo, likichelewa liache.

Ukitaka malizia, wengine watatibua,
Nia ukidhamiria, malengo utashikilia,
Pasiwe la kuhofia, kama lako hutimia,
Usilazimishe jambo, likichelewa liache.

No comments: