Wednesday, November 30, 2011

Haujaja

Mwenzio nilikungoja, usingizi haukuja,
Uliponiambia waja, nikasubiri kwa haja,
Umbeya kuubwabwaja,na maneno kuyafuja,
Uliniambia waja, mbona mwaya haujaja!

Uliogopa kufuja, vijisenti vya mseja,
Ujumbe niliungoja, simu ikaisha chaja,
Ikaondoka faraja, kwani wewe haujaja,
Uliniambia waja, mbona mwaya haujaja!

Linanisha daraja, kuvuka imesha haja,
Mie si mtu wa kungoja, kama vile kuna hoja,
Sipendi muda kufuja,majukumu yaningoja,
Uliniambia waja, mbona mwaya haujaja!

Pendo halijawa tija, kusubiri bila hoja,
Ningeliufunga mkaja,ningelipata mrija,
Soda nisingeifuja, ningeinywa kwa lahaja,
Uliniambia waja, mbona mwaya haujaja!

No comments: