Sunday, November 13, 2011

Mwandishi

Mwandishi kama silaha, adui ukimwachia,
Aweza kuitumia, wewe ukatokomea,
Wale wanaozubaa, fursa huiachia,
Mwandishi kama silaha, salama miliki wewe!

Mwerevu asipokuwa, watu watamtumia,
Kama chombo kutumiwa, ya kwao kutengenea,
Mwenyewe akabakia, hapo anapoachiwa,
Mwandishi kama silaha, salama miliki wewe!

Kumfundisha raia, ni kitu cha manufaa,
Sera akazielewa, na wito kuuchukua,
Kazi akasaidia, umma kujautetea,
Mwandishi kama silaha, salama miliki wewe!

Wale wanaoelewa, Che Guevara nakutajia,
Udaktari kaachia, uandishi kaingia,
Haya aliyatambua, na vyema kuyatumia,
Mwandishi kama silaha, salama miliki wewe!

Wakati umefikia, mapinduzi ya dunia,
Ukoloni kuukataa, wa nje na nyumbani pia,
Watu wetu kuokoa, maisha wakafurahia,
Mwandishi kama silaha, salama miliki wewe!

Na mengi kuazimia, daraja kujipandia,
Heshima kuichukua, dunia kututambua,
Nchi bora kuja kuwa, Afrika na dunia,
Mwandishi kama silaha, salama miliki wewe!

Inapasa kupangua, yale yasiyotufaa,
Na vyama kuvibagua, madhambi vilivyojaa,
Vyenye heri kuingia,habari zikaenea,
Mwandishi kama silaha, salama miliki wewe!

Wale wanaotumiwa, budi ngazi kuachia,
Mwende kwa yanayofaa, kizazi kukihurumia,
Wasije itwe mkaa, waache kuja kung'aa,
Mwandishi kama silaha, salama miliki wewe!

Uandishi ni sanaa, na wito wa kujaliwa,
Si kila mtu anajua, wengi wanajihadaa,
Huishia kutimiwa, fedha wakajagaiwa,
Mwandishi kama silaha, salama miliki wewe!

Wengine wananunuliwa, magari kuwahadaa,
Na nyumba wenda kupewa, wito ukajasinyaa,
Pabaya wakaishia, wawe wasiojijua,
Mwandishi kama silaha, salama miliki wewe!

Mwandishi vitu hajawa, au kifaa kutumiwa,
Huyo anayetumiwa, kapotea tasnia,
Na njia ya kumuokoa, ni kumnyanyapaa,
Mwandishi kama silaha, salama miliki wewe!

No comments: