Sunday, November 27, 2011

Sura mbaya siioni

Kote nimeshaangalia, ni uzuri waenea,
Wakilishi watimia, hesabu haijapungua,
Waliokwishateuliwa, na ukubwa wakapewa,
Siioni sura mbaya, barazani kutokea.

Wakubwa wanachagua, malaika walokua,
Urulaini radhia, dunia waliopewa,
Watutungia sheria, mashaalah naitoa,
Siioni sura mbaya, barazani kutokea.

Ila ninavyojua, akili wanaojaliwa,
Sura hawajajaliwa, bahati ikitokea,
Ila mamisi najua, bandia washindiliwa,
Siioni sura mbaya, barazani kutokea.

Hili ninalishangaa, malaika walokua,
Nani anawachagua,kwa jinsi wafanania,
Utadhani pacha pia,kumbe hawana jamaa,
Siioni sura mbaya, barazani kutokea.

Sura mviringo hua, na umbo wastania,
Hakuna lakuzidia, na macho wamejaliwa,
Mwanamme huumia, sio changu nikijua,
Siioni sura mbaya, barazani kutokea.

Hawa ndio wanafaa, yetu kuzungumzia,
Au roho warushia, na pepo wazipepea,
Hili sipati kujua, ila wapo wanaojua,
Siioni sura mbaya, barazani kutokea.

Baraza imejaliwa, harufu za kuvutia,
Mavazi ya maridhia, kila rangi zinang'aa,
Ila hoja sijazijua,ukame nahisi kua,
Siioni sura mbaya, barazani kutokea.

Ila kuigilizia, hilo sijalibishia,
Na kasuku huambiwa, sawasawa kurudia,
Ni fotokopi murua, wakubwa kuzitumia,
Siioni sura mbaya, barazani kutokea.

Dada nawahurumia, sura wasiojaliwa,
Chama hiki mtaloa,hawatawafikiria,
Sura usipojaliwa,kingine ni kuhamia,
Siioni sura mbaya, barazani kutokea.

Nyie wenye sura mbaya, undeni chama kipya,
Huenda mkatokea, nafasi kuichukua,
Ya haki iliyokuwa, na wala si ya kupewa,
Siioni sura mbaya, barazani kutokea.

Macho nimewafumbua, wenyewe kuogelea,
Bahari wametifua, majini waso shujaa,
Nuksi zakaribia, lazima kuwashtua,
Siioni sura mbaya, barazani kutokea.

No comments: