Wednesday, November 30, 2011

KIpaumbele

Nchi imeshaamua, magari kwanza kutua,
Nchini yakaenea, mitaani yakajaa,
Ili watu kudhania, nchi inaendelea,
Barabara zije mwisho, magari tulete kwanza!

Mjinga hajatambua, nafasi kaitumia,
Garii pato lagombea, na wake hao jamaa,
Petroli likajaa, na watu kulala nja,
Barabara zije mwisho, magari tulete kwanza!

Ufahari wakolea, wajivuna kwenye njia,
Mfukoni ukiingia, ndururu haijasalia,
Eti huku kwendelea, kwa vipi sijajua,
Barabara zije mwisho, magari tulete kwanza!

Magari hutangulia, barabara kufatia,
Ni sheria yabuniwa, kitini waliokaa,
Mwehu wanamdhania, mwalimu kuvikataa,
Barabara zije mwisho, magari tulete kwanza!

Utu umewapotea, watazame kwenye njia,
Kila anayetumia, ataka wa kwanza kua,
Na haya yakitokea, wote huwa wachelewa,
Barabara zije mwisho, magari tulete kwanza!

Kwa mguu wanaotembea, vigumu kuheshimiwa,
Wajinga wanaambiwa, na matusi kutupiwa,
Ma'na walojaliwa, ndio wenye motokaa,
Barabara zije mwisho, magari tulete kwanza!

Pikipiki nazo pia, Bajaji zinafuatia,
Ubinadamu wapea, majiani ni balaa,
Watalii wakimbia, salama imepotea,
Barabara zije mwisho, magari tulete kwanza!

Kwenye hizi zetu njia, kama hakuna sheria,
Wenyewe wajiamulia, wanalolifikiria,
Na hata wakikosea, rushwa wanaitoa,
Barabara zije mwisho, magari tulete kwanza!

Polisi waangalia, wazidi changanyikwa,
Nani kumshikilia, nani kumuachia?
Imekua kizaazaa,kwenda nje kutembea,
Barabara zije mwisho, magari tulete kwanza!

Ila wanapoambiwa, virungu kuturushia,
Haraka huchangamkia, ila kuja tuibia,
Mradi umeshakua, walo juu hawajajua,
Barabara zije mwisho, magari tulete kwanza!

No comments: