Wednesday, November 30, 2011

Shoka hataki kazi

Shoka kakataa kazi, kukiondoa kisiki,
Kasema huyu hamwezi, kiuno hakishikiki,
Amemzidi ujuzi, na tena hatabiriki,
Shoka kakataa kazi, ya kisiki cha mpingo.

Kagundua pingamizi, kisiki hakikatiki,
Litamchosha mkwezi, mwenye afya ya kaniki,
Hata na wao Maswezi, hili hawaaminiki,
Shoka kakataa kazi, ya kisiki cha mpingo.

Hautambi ujuzi, hakina mpango kisiki,
Hukufanya mpuuzi, watazame Wagiriki,
Hata ufanye zoezi, ukija kwaye hacheki,
Shoka kakataa kazi, ya kisiki cha mpingo.

Hili kubwa dudumizi, kung'oka haliafiki,
Wanageuzwa machizi, wakijaribu hilaki,
Hutiririka machozi, mahala hapakaliki,
Shoka kakataa kazi, ya kisiki cha mpingo.

No comments: