Sunday, November 13, 2011

Tanzania ni nyingine

Tanzania ni nyingine

Ni nyingine Tanzania, jana, juzi haijawa,
Macho wameyafungua, kusinzia walokua,
Kuamka wadhamiria, vigumu kuwahadaa,
Tanzania ni nyingine, siyo ya jana na juzi!

Vyombo wametunukiwa, ukweli vyawaambia,
Intaneti watumia, na hakika waijua,
Na kinachoendelea, siri zishafichuliwa,
Tanzania ni nyingine, siyo ya jana na juzi!

Chama kimoja wajua, ukiwa kimewatia,
Na mikataba kuzua, nchi iliyoiibia,
Ukiritimba unaa, ni nani asiyejua?
Tanzania ni nyingine, siyo ya jana na juzi!

Vyama vingi wanajua, si vita wala balaa,
Ni wachunga wengi kua, wezi waje kupungua,
Na kilio wakitoa, pawe wa kukipaazia,
Tanzania ni nyingine, siyo ya jana na juzi!

Vijana wamegundua, wazee kuwatumia,
Kwa malengo kujifaa, na sio ya wote wazawa,
Na sasa wanaamua, chama chao kujazua,
Tanzania ni nyingine, siyo ya jana na juzi!

Wanawake washangaa, waume kuwatumia,
Malengo wakafikia, nyuma wao wakabakia,
Na sasa washupalia, madaraka kuchukua,
Tanzania ni nyingine, siyo ya jana na juzi!

Polisi wanatambua, kazi kulinda raia,
Sio chama kusikia, na dhuluma kuingia,
Mahakama waijua, Hague inakokaa,
Tanzania ni nyingine, siyo ya jana na juzi!

Sisi sote ni wabia, wa nchi ya Tanzana,
Na wote kujatufaa, hiyo ndiyo yetu nia,
Hakuna wa kubagua, wala wa kupendelea,
Tanzania ni nyingine, siyo ya jana na juzi!

Mabomu yatapakaa, ya ajira na nazaa,
Kibiriti ukitoa, uwashapo angalia,
Na hata nao mshumaa, waweza zua balaa,
Tanzania ni nyingine, siyo ya jana na juzi!

Tamathali natumia, viongozi walokua,
Tenzi wanazozizua, tathmini kutumia,
Ili kutuepushia, tusiyo yatarajia,
Tanzania ni nyingine, siyo ya jana na juzi!

No comments: