Wednesday, November 30, 2011

Wazee wa Tanzania

Wazee mnatumiwa, kama fala mmekua,
Amkeni twawambia, asubuhi inshakua,
Yenu kusimamia, na sio kusimamiwa,
Wazee wa Tanzania, iundeni Jumuiya !

Wangapi wadhulumiwa, na yote tunayajua,
Serikali imekaa, pembeni yaangalia,
Vipi mwachaguliwa, harabu kuitikia?
Wazee wa Tanzania, iundeni Jumuiya !

Wazee mmejaliwa, busara zimewajaa,
Historia mwajua, na nchi ilikotokea,
Na tunakoelekea, mwaweza mkakosoa,
Wazee wa Tanzania, iundeni Jumuiya !

Na tunakoelekea, mwaweza mkakosoa,
Wakubwa kuwaambia, njia mmeshakosea,
Safari mkiendelea, lazima mtapotea,
Wazee wa Tanzania, iundeni Jumuiya !

Mkikubali kutumiwa, ni nani kuwaambia?
Wao watakujadhania, eti njia wanaijua,
Wakafosi kupotea, jahazi mrama likawa,
Wazee wa Tanzania, iundeni Jumuiya !

Wazee nawatambua, hekima mmeshapewa,
Mengi mmeshagundua, na wapi tunakosea,
Kussema mkijaliwa, wengi watayasikia,
Wazee wa Tanzania, iundeni Jumuiya !

Mkianza Jumuiya, haya kuzungumzia,
Pia itawatetea, na kilio kikasikiwa,
Adha zikawapungua, mkapata kupumua,
Wazee wa Tanzania, iundeni Jumuiya !

No comments: