Monday, November 21, 2011

Mchanga karata

ANA jozi ya pakiti, mchanga karata mwivi,
Anafanya tashtiti, wala sitii chumvi,
Twamtaka mwenyekiti, ambe aache ujuvi,
Mchanga karata mwivi, ana jozi ya pakiti.

Katufanya kaimati, hazigwai hata mvi,
Au sie matikiti, au mchana walevi,
Kikaagoni hauketi, hatujakua uduvi,
Mchanga karata mwivi, ana jozi ya pakiti.

Twamshikia manati, hayeeshi hivi hivi,
Kokoto tutamseti, aone mambo ni hevi,
Kweli hatumeremeti, ila hatunuki mavi,
Mchanga karata mwivi, ana jozi ya pakiti.

Yeye hatujamsaliti, wala kumwiita govi,
Vinginevyo hatupeti, twachanga bila ugomvi,
Mchanga karata mwivi, ana jozi ya pakiti.

Picha yake siipati, kisa yeye kuwa hivi,
Na maana haileti, naona geni jamvi,
Yumkini afriti,kampa wake ulevi,
Mchanga karata mwivi, ana jozi ya pakiti.

Alilolivaa koti, linalinda wake wivi,
Wadhani mtanashati, kumbe mkubwa mchimvi,
Keshabwagia na toti, chakari mpaka mvi,
Mchanga karata mwivi, ana jozi ya pakiti.

Achemshaye makuti, atambue hayaivi,
Na kiti ni cha kuketi, wala sio cha uvuvi,
Dogo wewe hulikuti, japo huanza kiwavi,
Mchanga karata mwivi, ana jozi ya pakiti.

Asemwe kwenye wavuti, wote wamjue mwivi,
Akakaa katikati, la ulimwengu jamvi,
Hata akiwa smati, atemee mate mwivi,
Mchanga karata mwivi, ana jozi ya pakiti.

Jumbe kichukue kiti, tumtete wetu mwivi,
Hata kama ana suti,isitufanye walevi,
Tumsute na kumseti, akomeshe wake wivi,
Mchanga karata mwivi, ana jozi ya pakiti.

No comments: