Sunday, November 13, 2011

Tatizo sasa si mtu

Leo si watu wabaya, ila yake mtu nia,
Na walioazimia, nchi yao kutumbua,
Na ukuu kupakua, ambao hawakupewa,
Tatizo leo si mtu, ni wakati umefika.

Hayo ndiyo yalokuwa, ya watu kuwashtua,
Ukweli wakaujua, na hali kuigundua,
Maamuzi kuchukua, kudhibiti kila njia
Tatizo leo si mtu, ni wakati umefika.

Ubinafsi kujaa, chini unamwagikia,
Kiasi kikizidia, balansi hupotea,
Sahani mbili kuliwa na mmoja haijatokea,
Tatizo leo si mtu, ni wakati umefika.

Uchama kuchuchumaa, siri kumezifichua,
Na wanaochungulia, kaburi wamegundua,
Wote,mwoga na shujaa, mauti kuwatembelea,
Tatizo leo si mtu, ni wakati umefika.

Akili wanaozidia, nchi hawataifaa,
Mikosi wataumua, nazaa pia balaa,
Mwishoni yatatokea, ya Syria na Libya,
Tatizo leo si mtu, ni wakati umefika.

Ufisadi kuenea, wezi wote tumekua,
Hata kwa wanaotujua, sasa wanatuchelea,
Maisha kizaazaa,nchi sasa imekua,
Tatizo leo si mtu, ni wakati umefika.

Bure utanichukia, si mimi ninayeamua,
Wakati umeazimia, na kengele inalia,
Yule asiyesikia, kiziwi ameshakua,
Tatizo leo si mtu, ni wakati umefika.

Mola kumgeukia, wakati umefikia,
Huenda akatuokoa, na kutuonesha njia,
Salama tukafikia, yote tulokusudia,
Tatizo leo si mtu, ni wakati umefika.

No comments: